KWA TAARIFA YAKO: MIAKA 7 YA KUKATALIWA KWA ASKOFU DUNSTAN MABOYA NA KUTOKA KWAKE T.A.G
![]() |
| Askofu mkuu wa CAG, Apostle Dunstan Maboya, akitoa salamu za rambi rambi kwenye msiba wa Askofu Moses Kulola jijini Mwanza hivi karibuni. |
Kwa waliokuwepo kipindi cha miaka ya tisini (wenye ufahamu wao), basi
jina la Mtume Dunstan Maboya linaweza lisiwe geni kwao, kwa ambao
wamekuwepo kuanzia milenia mpya (mwaka 2000), wanaweza wasifahamu fika
mtumishi huyu wa Mungu na mbeba maono wa Calvary Assemblies of God (CAG)
ni nani na alichopitia.
KWA TAARIFA YAKO ni kwamba Askofu Dunstan Maboya ndio mtu wa
kwanza kuitwa jina la mtume nchini Tanzania, na sio kwamba ilikuwa jambo
rahisi – ilikuwa ni kama mtu anayeonekana wa ajabu kuitwa hivyo, jambo
ambalo lilisababisha apigwe vita na watu kadhaa.
Mechanical Engineer huyu aliamua kuachana na taaluma yake na kuamua
kugeukia kuleta watu kwa Mungu mnamo miaka ya 70, na katika huduma yake –
alipewa nguvu ambazo, ilibidi apitie magumu kwa miaka 7 hadi kufanikiwa
(miaka ya mateso).
1981 ni mwaka ambapo kazi ilianza rasmi, mara baada ya Dunstan Maboya
kumaliza chuo cha thiolojia jijini Nairobi, na kuanza kazi na TAG.
Lakini katika makanisa yote ambayo alifanikiwa kufungua, ni maeneo
ambapo Moses Kulola alikuwa amefanya kazi na kufanya mageuzi makubwa,
kiasi cha kukubalika sana. KWA TAARIFA YAKO, mpasuko kati ya TAG
na EAGT ndio uliopeleka pia Dunstan Maboya kuonekana mtovu wa nidhamu
kutokana na kuishauri TAG iyaache makanisa yaliyofunguliwa chini ya
Kulola akiwa TAG, kwa kuwa alikuwa na kibali kuliko mtu yeyote. KWA TAARIFA YAKO, hapo ndio ikawa chanzo cha kuagwa na TAG, na kuelekea kuhudumu EAGT.
Mnamo 1990, Maboya alipata maono ya moja kwa moja ana kwa ana kutoka kwa
Mungu baada ya maombi makali na ya muda mrefu, na akaambiwa ya kwamba, “Nimekupa
Neema, ambayo Neema hii itakuwa ni kubwa na watu wengi sana watakuwa
wakifunguliwa bila kuwawekea mikono, na hao watu watadondoka na kupokea
uponyaji” lakini Mungu akamwambia kuwa Neema hiyo itaambatana na
watu kupinga na kwamba atapitia kwenye hali ngumu kwa kipindi cha miaka
7.
Hapo ndipo binadamu anabaki kuwa binadamu tu, maana KWA TAARIFA YAKO,
Mchungaji Dunstan Maboya alimkatalia Mungu, na kudai kwamba kama ni
hivyo hataki, na kwanini iwe yeye kupitia kwenye hali hiyo, ndipo jibu
la Mungu likatoka.
“Watu wote hawa ni watumishi wangu mimi, lakini nguvu hii kuibeba wengi hawawezi kustahimili mashambulizi yatakayotolewa” na kwamba Mungu anachotaka ni Neema hiyo ishuke maeneo mengi, na ndio itakayofanya kazi Afrika na duniani.
Baada ya makubaliano, akiwa Mbeya kwenye mkutano wa injili, akisema
Haleluya watui wanaanguka chini, hapo ndio ikawa mwanzo wa tatizo. Mnamo
miaka ya 90. “Huyu Maboya bwana haya maguvu anayotumia sio ya Mungu”
ndio maneno ya watu kipindi hicho. Lakini ni kipindi hicho hata injili
yenyewe ilikuwa ngumu, achilia mbali Neema iliyomshukia. KWA TAARIFA YAKO,
makanisa yote ya kiroho nchini yalimpinga isipokuwa Kanisa Katoliki, na
hata wahubiri wa makanisa ya Kiprotestant wakawa wanakemea ‘roho chafu’
iliyoingia ambayo inaitwa ‘power of god’.
“Mtu mwenyewe kijana mdogo tu, mhuni,” na matusi kedekede yaliporomoshwa
kwake. Hapo ndipo akasalimu amri na kumuambia Mungu kuwa huu mzigo
hautaki, lakini KWA TAARIFA YAKO jibu la Mungu kwake lilikuwa
kwamba aendelee tu. Kipindi cha miaka 7 hali hiyo iliendelea, ambapo
ilifikia hatua ya kukamatwa na kurudishwa kutoka nchi jirani kutokana na
namna alivyokuwa akitafsiriwa, hiyo ikiwa ni mwaka 1994.
Lakini KWA TAARIFA YAKO, hivi sasa ni amani na faraja tupu kwa
Askofu Dunstan Maboya akiona watu wanaombewa na kuanguka, kwa kuwa
anajua alikotokea, ilikuwa ni kupingwa kwa nguvu zote, lakini sasa hivi
inaonekana ni kawaida, anafurahia mabadiliko yaliyotokea kupitia kwake,
tofauti na kipindi ambacho ilikuwa watu wakianguka kwenye mikutano basi
inadaiwa ni nguvu za mapepo, na kugeuka chukizo mfano wa choo.
Vuguvugu hili la kukataliwa karibu kila sehemu, ndipo sasa KWA TAARIFA YAKO,
EAGT nao wakapata mashaka, na kumuondoa. Kuanzia hapo sasa akawa yupo
tu, na ndio ukawa mwanzo wa Calvary Assemblies of God mwaka 1992, na
kusajiliwa rasmi mwaka 1994, na kila aliyekuwa anamsupport akawa upande
wake na injili ikaendelea kama kawaida wakianzia Morogoro ambapo
makanisa takribani 40 yalifunguliwa, baada ya hapo akaelekea Arusha,
kasha Mwanza na kwingineko.
Hiyo KWA TAARIFA YAKO kama ulikuwa hujui kuhusu huduma ya
mtumishi wa Mungu, Askofu Dunstan Maboya na jinsi alivyoanza, kuna mengi
ameieleza Gospel Kitaa, endelea kutembelea nasi tutakuhabarisha mengine
zaidi, tukutane wiki ijayo.

0 maoni:
Chapisha Maoni