Yesu Anaponya.
Kama kuna kitu kinachowasumbua watu duniani ni matatizo
ya afya zao. Hata mataifa yaliyoendelea hayajaweza kuwahakikishia
raia wao usalama wa afya zao.
Kwa mataifa ya Afrika mambo ndiyo mabaya zaidi kwani
kuna uchache wa Mahospitali, Madaktari na Madawa. Umaskini nao ni
ukuta mwingine unaowazuia wengi kupata hizo huduma chache za Afya.
Pengine hii inachangiwa na Waafrika wenyewe kutotilia
maanani Madawa ya asili, na kuyakumbatia yale ya nchi za magharibi
ambayo hawawezi kuyagharamia, na wale wachache wanaoweza, wanajikuta
wakitumia madawa ambayo pengine muda wake wa kutumia umeisha, au ni
yale yanayofanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza, ambayo adhari zake
kwa mwanadamu hazijafaamika bado.
Upo ushahidi wa kutosha kuyatetea maoni yangu. Kwamba
katika enzi za mababu zetu kila ugonjwa ulitibiwa na aina fulani ya
mti shamba, na walikuwepo watu ambao kazi yao ilikuwa kuyafanyia utafiti
madawa hayo. Na kama watafiti hao wangeendelea mpaka leo, tungekuwa
na wanasayansi wetu ambao kugundua dawa ya ukimwi lisingekuwa tatizo
kwao.
Nisemalo ni hili, Mungu alipomuumba Mwanadamu alimwekea
duniani kila aina ya miti kwa matumizi mbalimbali na moja ya matumizi
hayo ilikuwa ni dawa. Kwa hiyo duniani kuna dawa za kutibu kila ugonjwa
pamoja na ugonjwa hatari wa dhambi, lakini cha ajabu wanadamu bado
wanaumwa na hawajui wapate wapi dawa. Kuendelea kuumwa wakati kuna
dawa, hilo siyo tatizo la Mungu, ila ni la Mwanadamu.
"Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekeza
watubu dhambi zao na kuniomba, Mimi nitasikia kutoka Mbinguni na kuiponya
nchi yao." Asema Bwana wa majeshi.
Wanadamu wakitubu na kuomba, ahadi ya Mungu ni kwamba,
atawaponya mahali popote walipo. Hii haijalishi kuwa wako Afrika au
Marekani. Mungu atatumia miti na utaalamu uliyoko Afrika kuwaponya
Waafrika na atafanya hivyo kwa watu wa mabara mengine. Sasa basi hakuna
haja ya kuogopa, kwani popote ulipo Mungu atatumia miti na utaalamu
wa hapo kukuponya.
Tatizo la Wanadamu ni kufikiri kuwa utaalamu wa bara
lingine ni bora kuliko ule wa kwao. Kwa sababu anayeponya ni Mungu,
na utaalamu pia unatoka kwake; Basi anaweza kuutumia utaalamu kidogo
kuuponya ugonjwa mkubwa, na pia kutumia utaalamu mkubwa kuponya ugonjwa
kidogo. Ili wale walio na utaalamu mkubwa wasiwe na la kujisifu.
Kwani adui mkubwa wa Mwanadamu ni maendeleo. Yeye
anafikiri anaendelea, kumbe ndiyo amejitengenezea tatizo la kummaliza
haraka. Aliyetengeneza ndege ndiye anaehitaji utaalamu wa kutengeneza
mahali pa kuiegesha hewani ili irekebishwe inapoharibika. Na yule
aliyetengeneza simu za mkono, ndiye anayehitaji hospitali kubwa kutibu
kansa ambayo inasababishwa na hizo simu za mkono.
Nataka kusema nini? Kwamba mengi ya magonjwa anayougua
mwanadamu leo amejitengenezea mwenyewe? ndiyo. Na hii ndio sababu
nchi zenye viwanda vingi, na magonjwa ni mengi kama viwanda vyenyewe.
Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake, ndiyo maana mtu naye ni muumbaji
wa namna yake. Tatizo ni kwamba Mwanadamu anaumba Gari ,analiendesha
akiwa mlevi, anasababisha ajali anaumia, halafu anamlaumu Mungu.
Mungu naye anashangaa !!! "Mimi nimempa uhuru wa
kufanya atakavyo, amejitengenezea umeme; Umeme umemchoma ananilaumu?
na mimi sijui umeme ni kitu gani, maana siyo moja ya vitu nilivyoviweka
ulimwenguni pale mwanzo."
Lakini kwa kuwa Mungu ni mwenye huruma nyingi, bado
tukimuomba atuponye anafanya hivyo. Na hatuwezi kumuomba uponyaji
wakati hatuamini kuwa yeye anaweza kufanya yale tunayomuomba. Kwanza
tunamwamini kupitia kwa Mwana wake Yesu kristo, pili tunamuomba atuponye
ugonjwa wowote; na Yeye atatumia njia yeyote kutuponya.
Niseme nini basi? Kwamba Mungu anaweza kuutumia
utaalamu wowote uliyoko Duniani kutuponya; Na sifa zisiende kwa wataalamu
bali kwa Mungu? Ndiyo! Kwani dunia na vyote vilivyoko ndani yake ni
mali ya Mungu. Utukufu una yeye milele na milele amina.
Basi sasa hakuna tofauti ya dawa za kienyeji na zile
zinazoitwa za kisasa, kwani Mungu huzitumia zote kuwaponya wanaomuomba
na kuzitumia. Na kwa wataalamu wanaowapa watu dawa, wajue siyo wao
wanaoponya, bali ni Mungu.
Kwa hiyo waache kuwatoza wagonjwa pesa nyingi.. Nanyi
wagonjwa mjue kuwa Mungu anaweza kuutumia utaalamu kidogo uliyoko
Afrika kuwaponya. kwa hiyo, siyo lazima kuharibu pesa kutafuta matibabu
ngambo kama alivyofanya Mobutu na baadaye akafa tu.
Nakumbuka kisa kimoja kinachomhusu mama yangu mzazi.
Alinitembelea Nairobi kutoka sehemu za mashambani nilikozaliwa, na
baada ya kukaa siku chache aliugua.
Na kama ilivyo kawaida ya wazee wengi, aliona atapona
tu bila kutumia dawa yeyote, lakini mambo hayakuwa hivyo kwake. Kwa
sababu alikuwa anaharisha, maji mwilini yalimwishia na tulipomfikisha
Hospitalini hali ilikuwa mbaya. Daktari akaamua alazwe.
Mambo yalianzia hapo, kwani kila muuguzi anapokuja
kumuuliza habari ya asubuhi, hizo ni shilingi elfu mbili na mia tano,
malipo ya salaam za asubuhi bila kuhesabu mchana jioni na usiku.
Baada ya siku tatu Hospitalini tulijikuta tunatakiwa
tulipe shilingi elfu arobaini. Kwa mshangao tulitaka tufahamishwe
pesa zote hizo ni za nini?
Ndipo tulipopewa orodha ya milo mitatu kwa siku,
japo mgonjwa mara nyingi alikuwa akikataa chakula.
Pamoja na elimu yangu ya msingi na n'gumbaru, nilichoweza
kuelewa kwenye hiyo orodha ni, Zile salamu za Daktari, na malipo ya
chakula asubuhi mchana na jioni. Mengine nilimwita kijana kutoka chuo
kikuu, naye akaweza kusoma zile gharama za kupima choo damu, pamoja
na kupima ubongo. Nyingine aliniambia kwa lugha ya kisomi kwamba ni
[tekniko] sana hata yeye haelewi ni nini
Ilitubidi tulipe elfu arobaini shilingi za Kenya,
na tukamwomba Mungu atulinde, janga la kulazwa hospitalini lisije
likatufika tena.
Na kila siku tunamshukuru Mungu kwa ulinzi wake maishani
mwetu na tunawaombea wale ambao hawajamjua Mungu na uponyaji wake,
wamjue sasa. kwani kumjua Yesu ni uzima.
Imeandikwa na Hezzo Daking mtumishi wa mungu
0 maoni:
Chapisha Maoni