ASKOFU MKUU WA KANISA LA TAG DK. BARNABAS MTOKAMBALI ASIFU NJOMBE KUONYESHA MFANO
Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Dk. Barnabas
Mtokambali, ametoa rai kwa maaskofu nchini, kuiga mfano wa ujenzi wa
chuo cha kupanda makanisa kilichopo Njombe ili kutimiza mpango mkakati
wa “Miaka Kumi ya Mavuno Tanzania kwa Yesu.”
Dk. Mtokambali alitoa nasaha hizo wakati wa mahafali na uzinduzi wa chuo
cha kupanda makanisa kilichopo Mkoa wa Njombe, chini ya Askofu wa Jimbo
hilo, Patrick Luhwago, sanjari na semina elekezi ya viongozi
iliyomalizika Juni 28, 2013.
Askofu huyo alinasihi watumishi kujituma na kukamilisha ujenzi wa vyuo
vyao vya kupanda makanisa, vilivyomo majimboni mwao ili kupata watenda
kazi wengi walioandaliwa kiufanisi katika shamba la Bwana.
Akihutubia katika uzinduzi huo, Dk. Mtokambali alieleza sababu za msingi
za kuanzisha vyuo hivyo vya kupanda makanisa kote nchini kuwa ni pamoja
na Kanisa kuongezeka kiidadi kupitia watendakazi wengi walioandaliwa
vya kutosha na vyuo hivyo.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni Kanisa la TAG kukua kijografia, kiasi
cha kufikia maeneo ambayo hayajafikiwa na injili, hivyo kulifanya kukua
kwa kasi kama ilivyokuwa enzi za kanisa la Matendo ya Mitume ambalo
Yesu aliliacha duniani.
“Kuna ulazima mkubwa kwa kanisa letu kukua kijiografia hata kuwafikia
watu ambao hawajawahi kufikiwa na injili,” alisema Dkt. Mtokambali.
Alieleza sababu zingine za kuanzisha vyuo hivyo kuwa ni pamoja na
kuliwezesha kanisa kukua kiufanisi na kwa ubora kama Neno la Mungu
linavyoagiza.
“Mshirika yeyote wa kanisa la mahali pamoja, mwenye wito wa kufanya kazi
ya Mungu ni vema akapitia chuo cha kupanda makanisa na kupata cheti cha
utendakazi, huku akiwa na elimu nzuri na mafunzo sahihi. Itamrahisishia
kutenda kazi kiufanisi wakati wa huduma mahali popote tofauti na hapo
awali,” alisema Dkt. Mtokambali na kuongeza:
“Watu walikua wanaenda kutumika kabla hata ya kupata mafunzo ya utumishi
na hatimaye kupata watu ambao wanaenda kinyume na misingi ya Neno la
Mungu.”
Kutumia vema rasilimali ya Kanisa la TAG, ni miongoni mwa sababu
aliyoitaja huku akiongeza kuwa, kwakua kila kanisa la mahali pamoja
hutoa asilimia 5, kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya kutegemeza vyuo
hivyo vya Biblia.
Aliongeza kuwa, asilimia 75 hutoka makao makuu kwaajili yakutegemeza
vyuo hivyo, na kusema TAG imewekeza kwa watumishi wake wote wanaopitia
vyuo vya Biblia nchini Tanzania; huku akisisitiza kwa wale ambao
wanasoma vyuo hivyo na kutoingia shambani kwaajili ya utendaji kazi,
hawawatendei haki washirika wa TAG wanaojitoa kwa mali zao.
Sanjali na hayo, Dkt. Mtokambali aliongeza sababu zingine kuwa ni
kufanya jimbo kuwa na kituo chake kwa ajili ya shughuli za kijimbo,
hapo ndipo patakua sehemu sahihi ya kufanyia mikutano, semina, makambi
na mambo yote yahusianayo na jimbo kuliko kukodisha kumbi sehemu
zingine.
Aidha Askofu alisisitiza kuwa kuna vijiji vingi ambavyo bado
havijafikiwa na injili, huku kanisa la Bwana likiwa limeridhika kwa kazi
za pale kanisani tu, bila kupeleka injili mahali ambapo bado
hapajafikiwa ambapo alihoji:
“Kwanini vinywaji vya soda kama vile cocacola, pepsi na vinginevyo
vimefika?. Hata vyama vya siasa huko ambapo injili bado haijafika
vyenyewe tayari vimeshafika, kwanini kanisa tumelala na kutokuthamini
kusudi la Mungu alilotuokoa kwalo?” alihoji kwa uchungu na kuongeza:
“Kama vinywaji vimefika pamoja na vyama vya siasa, basi Yesu wetu ni
zaidi ya hivyo vyote, jina lake lastahili pekee kusikika Tanzania yote.”
Kwa upande wa mgeni kutoka nchini Marekani, Mch. David Willington
aliwaasa watumishi kutokukata tamaa, kuvunjika moyo, kujikinai kwa yale
wanayopitia na badala yake watambue kuwa katika changamoto zote
wanazozipitia bado Mungu yu pamoja nao, na kuwa vita vya huduma zao si
wao watakaopigana bali Mungu aliyewaita.
You might also like:
0 maoni:
Chapisha Maoni